Wednesday, October 13, 2010

MENGI AFICHUA NJAMA ZA POLISI KUMBAMBIKA MWANAYE 'UNGA'


Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi.

Maofisa waandamizi watatu wa Jeshi la Polisi nchini wakiwepo wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya pamoja kile cha kimataifa (Interpol), wameingia dosari baada ya baadhi ya maofisa wake kudaiwa kutaka kumbambikia dawa za kulevya mtoto wa kiume wa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi.

Mkuu wa Kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa, na baadhi ya maofisa wa polisi akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO), Charles Mkumbo, wamedaiwa kuhusika katika mchezo huo mchafu wa kutaka kumwekea dawa za kulevya mtoto huyo, Abdiel Mengi, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mengi alisema tukio hilo lilitokea Septemba 26, mwaka huu siku mwanaye (Abdiel), alipanga kusafiri kwenda nchini India kikazi.

Mengi ambaye alizungumza kwa majonzi makubwa, alisema kwa bahati nzuri, Abdiel alilazimika kuahirisha safari ndipo mchezo huo uliposhindwa kufanikiwa, lakini vigogo hao walikuwa wameshapokea nusu ya malipo ya kazi hiyo.

Alisema Kamishna Nzowa, Kamanda Mkumbo na ofisa mmoja wa kitengo cha Interpol ambaye alimtaja kwa jina moja la Henry, waliahidiwa donge la Dola za Marekani 40,000 wakati vijana wawili ambao ni wafanyakazi wa uwanja wa ndege waliahidiwa Sh. milioni 15 kila mmoja.

Mengi alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, alilazimika kufuatilia tukio hilo kwa kina na kubaini kuwa maofisa hao walipokea nusu ya malipo ambayo ni Dola za Marekani 20,000 kila mmoja wakati vijana wa uwanja wa ndege walipewa Sh. milioni saba kila mmoja.

Alisema mchezo huo ulimhusisha pia kijana mmoja ambaye anafanya kazi katika moja ya kampuni za simu nchini ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina.

Alisema kijana huyo naye aliahidiwa Sh. milioni 15 na kwamba alipewa Sh. milioni saba kama malipo ya awali.

“Niseme tu kwamba naridhika sana na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi na tunaweza kujivunia utendaji wa viongozi wa Jeshi hilo kama IGP, Said Mwema, Kamanda Venance Tossi, Kamanda Suleiman Kova, Kamanda Elias Kalinga, Kamanda David Nisile, Shilogile na wengineo wanaolitumikia Jeshi hilo kwa nguvu zao zote na kwa uwezo mkubwa,” alisema.

“Lakini kwa bahati mbaya kuna viongozi wachache katika Jeshi la Polisi ambao wanaharibu sifa nzuri ya Jeshi hilo, wanaweza kuliletea Jeshi letu sifa mbaya hapa na pale...ni kwanini nimesema hivyo, nitoe mfano mmoja hai unaoonyesha viongozi wachache ndani ya Jeshi hilo wanavyoweza kufanya jeshi la polisi lionekane halifanyi kazi vizuri,” alisema Mengi.

Alisema: “Tarehe 26, Septemba, mtoto wangu anaitwa Abdiel alipanga kwenda India kikazi pamoja na marafiki zake watatu, lakini kwa bahati nzuri tulielezwa kwamba kulikuwa na mpango wa kumbambikia madawa ya kulevya na kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliweza kuahirisha safari yake.”

Alisema anavyomfahamu mtoto wake, ni kijana mwadilifu asiye na tabia mbaya hususani kujihusisha na dawa za kulevya.

Alisema viongozi waliohusika katika mchezo huo wameonyesha jinsi ambavyo sio waadilifu katika kuwatumikia wananchi.

Mengi alisema uchunguzi wake umebaini kwamba mchezo huo uligharimiwa na mmoja wa wafanyabiashara ambao aliwahi kuwataja kama mafisadi papa, wanaohusika katika ufisadi mkubwa nchini.

Alisema uchunguzi wake umebaini pia kwamba mchezo huo mchafu ulitengewa Sh. bilioni tatu.

“Ushauri wangu, nadhani hawa watu hasa walioko Polisi hawapaswi kuwa pale, ni watu waovu hawajali mateso ya wenzao...this is more inhuman (hii ni kukosa utu) huwezi kusema hii ni rushwa, ushauri wangu ni kwamba waachie ngazi waondoke jeshini halafu kama ni Mwislam aende msikitini kutubu, Mkristo aende kanisani kutubu, wamrudie Mwenyezi Mungu,” alisema Mengi.

Alisema iwapo vigogo hao wataona wameonewa, wanaweza kwenda mahakamani ili mchezo mzima ujulikane huko.

“Kwa kuwa nchi yetu inazingatia utawala wa kisheria, nadhani wataenda mahakamani watashtaki kwa kuwachafulia majina, nimejiandaa, nina uhakika hata wao wamejiandaa, kama wanataka kuumbuka zaidi,” alisema.

Akizungumzia tuhuma hizo, Kamishna Nzowa, alishangaa kuhusishwa na tukio hilo na kueleza kwamba hamfahamu Mengi wala Abdiel na kwamba kamwe hajawahi kuchukua fedha kwa nia ya kumbambikia mtu madawa ya kulevya.

“Hiyo tarehe yenyewe unayoitaja mimi nilikuwa Ethiopia na unajua mimi sio mwanasiasa wala mfanyabiashara, ningefanya hivyo kwa interest (maslahi) ya nani?” alihoji na kuongeza:

“Simfahamu Mengi na nina uhakika pia yeye hanifahamu, maana ingekuwa tunafahamiana ningesema pengine tulikorofishana sehemu fulani.”

Alisema hivi karibuni, kitengo chake kilikamata dawa nyingi za kulevya mkoani Tanga na wahalifu walitaka kumhonga dola za Marekani 120,000, lakini akakataa kwa sababu anaiheshimu kazi yake.

“Itakuwa dola 40,000? lakini Biblia inasema wanaomtumainia Mungu hawataaibika milele, ukimcha Mungu hutaaibika...mimi sitaenda kushtaki mahakamani najua Mungu atawaumbua hao walionitungia uongo,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda Mkumbo alikana kuhusika na kusema kwamba: “Mimi ni ofisa mkubwa ndani ya jeshi siwezi kufanya hivyo kwa interest (maslahi) ya mtu...mtoto wa Mengi simfahamu, ila namjua baba yake kwa kumwona kwenye vyombo vya habari.”

“Sijui nitafanya nini, lakini nadhani Jeshi la Polisi (viongozi wangu), watafanya uchunguzi kubaini ukweli na Mengi atatoa vielelezo vyake, napenda kusema kwamba taarifa hizi ni za kughushi hazina ukweli wowote kwa asilimia 100,” alisema.

Kwa upande wake, Henry alipotafutwa simu yake haikupatikana jana.




CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment